KULA NYANYA
UJIEPUSHE NA KIHARUSI

SOTE tunajua ugonjwa wa kiharusi ( stroke)
ni miongoni mwa magonjwa hatari kwani
ukikupata unaweza kudhoofisha baadhi ya
viungo vyako vya mwili kama siyo vyote na
kukufanya ushindwe kufanya kazi zako za
kawaida na kuwa mtu wa ndani tu kwa
maisha yako yote.
Lakini unaweza kujiepusha na ugonjwa huo
hatari kwa kuzingatia ulaji wa vyakula sahihi
pamoja na kufanya mazoezi . Utafiti wa hivi
karibuni umebaini kwamba nyanya
( tomatoes) hutoa kinga mwilini dhidi ya
ugonjwa wa kiharusi au kupooza kama
unavyojulikana na wengine .
Hivi karibuni , watafiti wa nchini Finland
walifanya utafiti wa kina na kutoa taarifa
kuhusu kirutubisho aina ya ‘ lycopene’
kinachopatikana kwa wingi kwenye nyanya,
matikitimaji na pilipili . Wamesema katika
taarifa yao kuwa watu zaidi ya 1, 000
waliowafanyia utafiti wenye kiwango kingi
cha ‘ lycopene ’ kwenye mfumo wa damu zao,
hawakuonesha dalili kabisa za kupatwa na
kiharusi.
Aidha , Chama cha Taifa cha wenye Kiharusi
cha nchini Marekani ( The National Stroke
Association ) kimesema kuwa wanawake
wengi hufariki dunia nchini humo kutokana
na kiharusi kwa idadi sawa na wale
wanaofariki kutokana na ugonjwa wa
saratani ya matiti . Hii ina maana kwamba
ugonjwa wa kiharusi nao ni tishio kama ilivyo
kwa ugonjwa wa saratani ya matiti .
Utafiti mwingine katika eneo hilo umeonesha
pia kuwa wanaume wana hatari kubwa zaidi
ya kufariki dunia au kupatwa na matatizo
mengi kutokana na ugonjwa wa kiharusi
kuliko wanawake. Hivyo kati ya wanaume na
wanawake, wanaume zaidi ndiyo hupatwa na
kiharusi au matatizo yatokanayo na ugonjwa
huo kuliko wanawake.
Utafiti huu mpya umeendelea kuthibitisha
ukweli wa siku zote kuwa matunda na
mbogamboga hutoa kinga katika mwili wa
binadamu dhidi ya magonjwa mengi hatari ,
hivyo wito umetolewa tena wa watu kupenda
kula matunda na mbogamboga hasa nyanya,
matikitimaji pamoja na pilipili ambavyo
vimeonekana kuwa na kinga kubwa zaidi
mwilini .
Hata hivyo , imeelezwa kuwa baada ya
matokeo ya utafiti huu , watu
wamekumbushwa umuhimu wa kuendelea
kula na aina nyingine ya matunda , kwani kila
tunda au mboga ya majani ina faida na
umuhimu wake katika mwili wa binadamu.
Mwisho imeelezwa kuwa ulaji wa nyanya za
aina zote una faida , iwe ni ile inayopikwa
pamoja na mboga au ile inayoliwa ikiwa
imeiva bila kupikwa. Ni vizuri kuchangamkia
ulaji wa vitu kama hivi ili kuipa miili yetu
uwezo wa kujikinga wenyewe dhidi ya
maradhi hatari, yakiwemo yale ya saratani
ambayo kwa kiasi kikubwa huweza kuzuiwa
kwa kula mboga za majani na matunda ya
aina mbalimbali .

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni